SERIKALI IMESEMA HAITASITA KUVUNJA MKATABA NA KAMPUNI YA SKYWARDS CONSTRUCTION. | Yuvinusm-Habari Unazozitaka
Breaking News
Loading...

3/7/18

SERIKALI IMESEMA HAITASITA KUVUNJA MKATABA NA KAMPUNI YA SKYWARDS CONSTRUCTION.Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Wiliam Ole Nasha, amesema Serikali haitasita kuvunja Mkataba na Kampuni ya Skywards Construction
inayopaswa kujenga miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji katika Chuo cha Ualimu Ndala kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora.

Naibu Waziri ametoa Kauli hiyo baada ya Kampuni ya Skyward Construction iliyopaswa kujenga Mabweni, Vyumba vya Madarasa, Ukumbi, Maktaba, Maabara na Matundu ya vyoo kutoonekana katika eneo la ujenzi tangu alipokabidhiwa kutekeleza mradi huo mapema mwezi Januari 27, 2018.

Akizungumza akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi inayotekelezwa na Wizara yake kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matoke- EP4R, Naibu Waziri Ole Nasha amesema Kampuni hiyo tangu ikabidhiwe Mradi haijawahi kufika eneo la mradi kuanza ujenzi na bila taarifa yoyote hivyo kuacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu.

‘Kampuni hii ilipaswa kuanza kazi Februari 24, 2018 cha kushangaza hadi sasa haijaonekana eneo la Mradi bila taarifa yoyote. Kampuni hii ya Skyward Constuction inapaswa kujua imeingia mkataba na mikataba hii huwa ina taratibu zake, kama kuna jambo haliendi sawa ni bora akaeleza kwa kuwa Serikali haitasita kuvunja mkataba nae.’ Alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri Ole Nasha amezitaka Kampuni mbalimbali za ujenzi kuhakikisha zinazingatia Mikataba, kwani kuchelewa kukabidhi Mradi kwa wakati kunaisababishia Serikali gharama zisizo za lazima kwa kuwa vifaa vya ujenzi vitapanda bei lakini pia Mradi kushindwa kukidhi kusudio la kuwepo kwa wakati huo.

Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu Ndala Abinego Ndikumwe amesema pamoja na Serikali kukarabati na kujenga miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji bado Chuo hicho kina changamoto za upatikanaji wa Maji, ukosefu wa usafiri kwa matumizi ya Chuo, Bwalo na ofisi za Wafanyakazi.

Akiwa Wilayani Nzega Mhe. Ole Nasha ametemtembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Nzega na Mwanhala, Shule ya Sekondari Kampala na Shule ya Sekondari Mwanhala ambapo akiwa kwenye Shule ya Sekondari Mwanzoli na amekiri kurdhishwa na namna Shule hiyo ilivyotekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule, ambapo ameahidi Wizara yake itahakikisha inakamilisha ujenzi wa Maabara, na Nyumba mbili za Walimu.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

07/03/2018

Weka Maoni yako Hapa

google+

linkedin