Udom waanza kuufanyia kazi ushauri wa Mkapa | Yuvinusm-Habari Unazozitaka
Breaking News
Loading...

3/26/18

Udom waanza kuufanyia kazi ushauri wa Mkapa
Siku chache baada ya Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kutaka uwapo mjadala wa kitaifa wa hali ya elimu nchini, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimeanza kuufanyia kazi ushauri huo.


Machi 17, Rais huyo mstaafu alisema ipo haja ya kuitishwa mjadala wa kitaifa wa kujadili hali ya elimu kufuatia shule za Serikali kuendelea kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya Taifa.


Mkapa ambaye pia ni mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma aliyasema hayo mjini Dodoma wakati wa tukio la kumuingiza kazini makamu mkuu mpya wa chuo kikuu hicho, Profesa Egid Mubofu.


Kufuatia ushauri wake, jana Udom ilianza kuufanyia kazi kwa kukutana na makundi ya jamii kujadili elimu kwa watoto wenye ulemavu na kubaini upungufu katika utekelezaji wa sheria na sera.


Akizungumza jana, kaimu mkuu wa Chuo cha Elimu cha Udom, Dk Enedy Mlaki alisema mkutano huo uliojumuisha makundi mbalimbali ya kijamii ulilenga kusikia mawazo mbalimbali ya wadau wa elimu.


Alisema lengo ni kupata mawazo ambayo yatajenga mfumo mzima wa elimu jumuishi na hivyo kutowaacha nyuma watoto wenye ulemavu nchini. “Na kama mlivyosikia mwaka jana kuna shule moja kule Njombe wanafunzi karibu wote walifeli na sisi tukasema kama Chuo Kikuu cha Dodoma ambao tunaongoza kwa kutoa elimu bora tufanye kitu,” alisema Dk Mlaki.


Alisema wameamua kuchambua sera za elimu zinazohusu wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kupata mawazo ya makundi mengine ya jamii juu ya maeneo hayo.


Mkuu wa Idara ya Saikolojia wa Chuo cha Elimu katika Udom, Dk January Basela alisema Tanzania ina sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 na sheria inayoongoza huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2010.


Alisema sera iliyopo haijazungumza kwa upana juu ya majukumu ya kila Mtanzania katika kuhakikisha utekelezaji wa sheria na sera zilizotungwa.


“Lakini sera haifafanui ni kwa namna gani watu wenye ulemavu wanapata haki zao na huduma mbalimbali kama matibabu,” alisema Dk Basela.


Hata hivyo, alisema ingawa sera na sheria zimezungumzia huduma kwa walemavu, lakini hazijatekelezwa vizuri kama inavyotakiwa. “Kuna sheria zipo, kuna sera zipo lakini bado utekelezaji wake ni mgumu, hazijaweza kutekelezeka kwa kina inavyotakiwa,” alisema.


Dk Basela alishauri miundombinu ya elimu iwe rafiki ili kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kupata huduma na elimu.
Weka Maoni yako Hapa

google+

linkedin