Madudu zaidi yafichuliwa Bodi Mikopo Elimu ya Juu | Yuvinusm-Habari Unazozitaka
Breaking News
Loading...

4/15/18

Madudu zaidi yafichuliwa Bodi Mikopo Elimu ya JuuACHANA na kashfa ya kulipana posho ya ukarimu, madudu zaidi yamefichuliwa kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), safari hii Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikitakiwa kujitathmini kama kweli inastahili kuendelea kuisimamia bodi hiyo.Baada ya mwaka juzi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kubaini utafunaji wa fedha za HESLB kupitia utaratibu wa watumishi wake kulipwa posho mbalimbali, ikiwamo iliyoitwa posho ya uhusiano na ukarimu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) naye ameibua udhaifu mwingine wa kiutendaji katika bodi hiyo.

Miongoni mwa madudu yaliyobainishwa na CAG Prof. Mussa Juma Assad, ni kufikishwa mahakamani kwa wadaiwa sugu wawili tu katika kipindi cha miaka miwili ilhali taarifa zinaonyesha kuna wadaiwa sugu 163,394 wanaopaswa kuchukuliwa hatua hizo za kisheria.

CAG pia amebaini bodi hiyo haina uwezo wa kuwapatia mikopo wanafunzi wote wenye sifa bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini pamoja na changamoto ya ulipaji fedha hizo kwa wahitaji.

Katika ripoti yake ya Ukaguzi wa Ufanisi katika Usimamizi wa Urejeshaji wa Mikopo na Ukusanyaji wa Madeni ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini aliyoiwasilisha bungeni wiki hii, Prof. Assad anabainisha kuwa, amegundua urejeshaji wa mikopo na ukusanyaji wa madeni kwa kipindi cha kuanzia 2012/13 hadi 2016/17 ni chini ya asilimia 50 ya mikopo iliyoiva.

Alisema bodi hiyo haikuweza kufikia lengo lake la makusanyo ya mikopo katika kipindi hicho cha miaka mitano.

"Tathmini ya utendaji ilionyesha kuwa makusanyo ya kila mwaka ya mikopo iliyoiva ya wanafunzi wa elimu ya juu yaliyokokotolewa kutoka kwenye takwimu za jumla za makusanyo yalikuwa kati ya asilimia 32 na 48 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2012/13 hadi 2016/17," Prof. Assad anaeleza katika ripoti yake hiyo.

Anabainisha kuwa kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2016/17, makusanyo kwa mwaka yaliongezeka kutoka Sh. bilioni 28 hadi bilioni 116, ikilinganishwa na kipindi cha kati ya mwaka wa fedha 2012/13 na 2014/15, ambacho makusanyo kwa mwaka yalikuwa kati ya Sh. bilioni 15 na bilioni 22.

Anasema miongoni mwa sababu za ongezeko hilo ikilinganishwa na miaka ya nyuma ni jitihada zilizofanywa na menejimenti ya bodi katika kipindi hicho.

Hata hivyo, Prof. Assad anabainisha kuwa pamoja na jitihada hizo, bado urejeshaji wa mikopo na ukusanyaji wa jumla ya madeni ya mikopo ulikuwa chini ya lengo lililowekwa. 

Anaeleza kuwa ukaguzi wake ulibaini kuwa makusanyo hafifu yalichangiwa na udhaifu katika uandaaji na utekelezaji wa mikakati ya kuwabaini na kuwadai wanufaika wa mikopo pamoja na ufuatiliaji na tathmini hafifu ya utendaji wa bodi na Wizara ya Elimu.

Anasema shughuli za kuwabaini na kuwadai wanufaika wa mikopo hazikufanyika ipasavyo kwa kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kiwango cha kuwabini wanufaika wapya kwa kigezo cha mikopo iliyoiva kimeongezeka kutoka asilimia 28 hadi 58 ya wanufaika kwa kipindi cha mwaka 2013/14 hadi 2016/17.

Hata hivyo, CAG Assad anasema ongezeko halikuwa sawa na idadi ya wanufaika wa mikopo iliyoiva, akitolea mfano idadi iliyoongezeka kwa kiasi kikubwa katika mwaka wa fedha 2016/17 hadi kufikia asilimia 51 ikilinganishwa na miaka iliyopita.

"Miongoni mwa sababu zilizochangia udhaifu katika kubaini wanufaika wa mikopo ilikuwa ni upungufu katika kupanga na kutoa taarifa ya ukaguzi za kuwabaini wanufaika wa mikopo," CAG anasema na kuongeza: 

"HESLB haikuwa na mpango wa ukaguzi kwa kipindi cha miaka minne ya fedha, yaani kutoka 2012/13 hadi 2015/16. Ukaguzi ulibaini kuwa ingawa bodi iliandaa mpango wa ukaguzi wa wanufaika wa mikopo kwa mwaka wa fedha 2016/17, hapakuwa na taarifa za utekelezaji wake zilizowasilishwa kwa menejimenti ya bodi."

Prof. Assad pia anabainisha kuwa kulikuwa na udhaifu katika kuwadai wanufaika wa mikopo waliokuwa wanalipwa mishahara na serikali.

Anasema uchambuzi wake wa sampuli ya taarifa ya wafanyakazi 180 kati ya 15,885 walionufaika na mikopo kutoka katika mfumo wa ulipaji mishahara serikalini, ulibaini wanufaika 135 hawakuwa wamepelekewa kikamilifu ankara za madai yao ya HESLB.

"Hii ni kwa sababu mfumo wa kuchakata mishahara serikalini ulionyesha kuwa wanufaika husika hawadaiwi baada ya makato yaliyokuwa yamefanyika kwa mujibu wa taarifa zilizopelekwa na HESLB wakati kwa upande wa bodi hiyo wadaiwa hawa 135 walikuwa na deni la Sh. milioni 362," anabainisha.

WAWILI TU KORTINI 

CAG Assad pia anaeleza kuwa, amebaini kuna udhaifu katika uchukuaji wa hatua dhidi ya wadaiwa sugu wa madeni ya mikopo.

Anasema wakati wa ukaguzi bodi hiyo ilikuwa na wadaiwa sugu 163,394, lakini kumbukumbu za bodi zilizowasilishwa kwa wakaguzi zilionyesha kulikuwa na wadaiwa sugu 18.

Pia CAG anaeleza kuwa kumbukumbu zilionyesha kuwa ni wadaiwa sugu wawili tu ndio waliofikishwa mahakamani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

"Zaidi ya hapo, kulikuwa na waajiri 70 ambao walishtakiwa ama kwa kuchelewesha makato ya mkopo au malipo ya madeni ya mikopo waliyokusanya. Jumla ya faini iliyotozwa kwa waajiri wote 70 ilifikia Sh. milioni 267.5 ingawa bodi ilikusanya Sh. milioni 57 sawa na asilimia 21 tu ya faini hizo kutoka kwa waajiri," alisema. 

MAPENDEKEZO

CAG Assad anasema taarifa za HESLB zinaonyesha mwaka 2016/17, ni wanafunzi 28,383 tu kati ya 48,502 (asilimia 58.5) waliostahiki kupata mikopo kulingana na vigezo, walipewa mikopo kutokana na uwezo mdogo wa bodi hiyo kutoa mikopo.

Kutokana na udhaifu huo, Prof. Assad anapendekeza HESLB inapaswa kuandaa kanzidata ya wanufaika wa mikopo yenye viashiria vya hatari na kuiunganisha na mikakati ya urejeshaji wa mikopo na ulipaji wa madeni ya mikopo ili kuongeza ufanisi katika ugawaji na matumizi ya rasilimali hasa katika kubaini wanufaikawa mikopo.

Pia anapendekeza bodi hiyo kutumia teknolojia inayofaa kama vile malipo kwa njia ya simu ili kurahisisha mchakato wa urejeshaji wa mikopo na ulipaji madeni ya mikopo na urahisi wa upatikanaji wa taarifa za mkopo kama vile salio la mkopo na tozo zingine kama vile faini.

Prof. Assad pia anapendekeza bodi hiyo kutambua na kuchukua hatua za kisheria mara kwa mara dhidi ya wadaiwa sugu na wanufaika wanaokiuka masharti ya ulipaji mikopo ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadhamini na waajiri wao.

"Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapawa kujitathmini kama ina uwezo wa kuendelea kusimamia utendaji wa moja kwa moja wa HESLB katika kushughulikia urejeshaji wa mikopo na ukusanyaji wa madeni ya mikopo ama kuipa kazi taasisi nyingine ya serikali kama vile Wizara ya Fedha na Mipango yenye ujuzi na uzoefu wa masuala hayo," CAG anapendekeza.

Mwaka juzi, PAC ilipokuwa inapitia hesabu za HESLB bungeni mjini hapa, ilibaini utafunaji wa mabilioni ya shilingi uliokuwa unafanywa na watendaji wa bodi hiyo kupitia njia mbalimbali zikiwamo za kulipana posho za safari za ndani na nje ya nchi, posho za kufiwa, posho ya uhusiano na ukarimu na mwanafunzi mmoja kuwekewa fedha za mikopo ya wanafunzi wengine.

chanzo: Nipashe
Weka Maoni yako Hapa

google+

linkedin