Mabilioni Yayeyuka Sekta ya madini | Yuvinusm-Habari Unazozitaka
Breaking News
Loading...

5/1/18

Mabilioni Yayeyuka Sekta ya madini


WAZIRI wa Madini, Angella Kairuki, amewaagiza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), kuchunguza upotevu wa zaidi ya Sh. bilioni 30 unaodaiwa kuwamo katika fedha za kodi zilizotolewa na kampuni za madini, mafuta na gesi kwa mwaka wa fedha 2015/16.


Kampuni 55 kati ya 1,287 za madini, mafuta na gesi zililipa kodi ya jumla ya Sh. bilioni 465.164 kwa mwaka 2015/16, lakini zilizopokewa serikalini ni Sh. bilioni 434.627 tu.

Waziri Kairuki alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kuzindua Ripoti ya Nane ya Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia nchini (Teiti).

Kadhalika, ripoti hiyo imeonyesha kuwa kati ya kampuni hizo 1,287, kampuni 55 zilichangia asilimia 95.05 za makusanyo na kampuni 1,232 zilichangia asilimia 4.95 ya makusanyo yake.

Kairuki aliipongeza Teiti kwa kazi nzuri iliyofanya na kusisitiza kuwa lazima ifahamike sababu za kujitokeza kwa tofauti hiyo ya fedha.

"Natoa maelekezo kuwa ripoti hii ipelekwe kwa CAG kwa ajili ya uchunguzi kama kifungu 18(1) cha Sheria ya Teiti ya mwaka 2015 kinavyotaka. Tunataka ripoti hii iende kwa CAG, ili tujue nini kimetokea na ni vyema kazi hiyo ikafanyika kwa wakati,"alisema.

Pia alisema ripoti hiyo inaonyesha sekta ya madini imechangia kwa asilimia 85 na sekta ya mafuta na gesi asilimia 15 ya mapato ya serikali kwa mwaka 2015/16. 

Kuhusu mapendekezo ya kamati ya Teiti, alisema yatafanyiwa kazi kwa haraka kwa maslahi ya Watanzania wote.

Kairuki alisema Tanzania ilijiunga katika mpango wa kimataifa wa uwazi katika sekta ya uchimbaji wa rasilimali kwa lengo la kuhakikisha mapato yake yanafahamika bila kificho.

"Hivyo serikali na kampuni za madini zina jukumu la kutoa taarifa zao kuhusu kilichopatikana katika uchimbaji wa madini, mafuta na gesi katika kipindi husika. Nichukue fursa hii kuipongeza Teiti kwa kazi nzuri ambayo wameifanya tangu mwaka 2001 walipoandaa taarifa ya kwanza hadi leo hii tumefikia kuzindua taarifa ya nane," alisema Kairuki.

Naye Msimamizi wa Kujitegemea wa Teiti aliyewasilisha ripoti hiyo, Simphorian Malingumu, alisema malipo ya mrabaha wa madini yalichangia asilimia 36 ya makusanyo kutoka rasilimali ya madini, mafuta na gesi asilia.

Alisema kampuni iliyolipa kodi kwa kiwango kikubwa ni Geita Gold Mine (GGM) ambayo ililipa asilimia 46.92, Bulyanhulu asilimia 9.72, Pan African Energy asilimia 9.66 na North Mara asilimia 9.26.

Kadhalika alitoa mapendekezo ya Teiti kuboresha orodha ya leseni za madini kwa kuingiza taarifa zote za wamiliki.

Mapendekezo mengine ni kuanzisha orodha ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na Wizara ya Madini kuweka kumbukumbu sahihi za malipo ya ada na mrabaha kwa kuzingatia wamiliki wa leseni.

Wakati huo huo, Kamati ya Taasisi za Kiraia zilizomo Teiti, zimeitaka serikali kutoa ripoti mapema na kuweka katika lugha rahisi, ili iwafikie wananchi kwa urahisi zaidi.

Mjumbe wa Kamati hiyo, Grace Masalakulengwa, alisema pia kamati hiyo iwe na mwenyekiti rasmi badala ya aliyepo kuendelea kukaimu kwa muda mrefu.

"Serikali itoa muda wa kutoa elimu kwa wadau hasa kampuni za sekta ya madini, mafuta na gesi kuhusu kazi za Teiti na umuhimu wake maana kuna sehemu nyingine tunaingia watu wanatushangaa," alisema Masalakulangwa ambaye pia anawakilisha kundi la taasisi za dini katika kamati hiyo.

Pia waliishauri serikali kutumia fedha za kodi kuendeleza rasilimali za nchi badala ya kuzitumika katika bajeti ya kitaifa.

"Rasilimali za madini, mafuta na gesi ni muhimu ambazo zinapotea hivyo ni vyema sasa serikali ikaendeleza rasilimali muhimu kama hizi, ili kuwe na kitu cha kujivunia kama taifa kupitia kodi hizi," alisema

#NIPASHE
Weka Maoni yako Hapa

google+

linkedin